1.5 Maombi katika Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika (KJSA)
Katika miaka ya hivi karibuni, teknolojia nyingi zimeonekana kwenye soko ambapo zimekusudiwa kusaidia katika sekta za afya na huduma za utengamao. Aina za teknolojia hazina kikomo, kwani kampuni za teknolojia zinaweza kuunda teknolojia zinazokidhi karibu mahitaji yoyote ya mteja kwa kutumia teknolojia mpya au iliyosasishwa. Katika sura ya 6, utajifunza kuhusu teknolojia za kidijitali zinazotumika zaidi katika huduma za utengamao. Uwezo wa teknolojia za kidijitali ni muhimu sana katika utoaji wa huduma za afya sio tu katika muktadha wa kimataifa bali pia katika nchi zenye kipato cha chini. Miongoni mwa vipengele vingine, teknolojia za kidijitali pia zina uwezo wa kutoa huduma za utengamao kwa watu wanaoishi vijijini na maeneo ya mbali katika nchi zinazoendelea. Teknolojia za kidijitali sio muhimu tu katika kuboresha huduma za afya lakini pia ni bora katika mifumo ya afya ili kufikia malengo ya huduma ya afya kwa wote iliyofafanuliwa na Shirika la Afya Duniani (SAD) (tazama sura ndogo 1.2. kwa uwezekano zaidi wa Huduma ya Utengamao Kidijitali).
Inaripotiwa kuwa huduma za afya ya simu zaidi ya 1000 kwa sasa hutoa maelezo ya afya na huduma za uchunguzi katika nchi za kipato cha chini [14]. Suluhu za kidijitali zimezidi kuwa maarufu kwani watu wengi zaidi wanamiliki simu za rununu. Kwa mfano, watu milioni 414.77 katika Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika (KJSA) walijiandikisha kupokea simu janja mwaka wa 2022, kutoka watu milioni 118.1 mwaka wa 2015 [15]. Kwa kuongezea, ufikiaji wa mtandao umeboreshwa. Mtandao mpana wa rununu sasa unashughulikia maeneo mengi ya mijini. Mnamo 2021, 83% ya idadi ya watu wa KJSA waliishi katika eneo lililofunikwa na mtandao mpana wa simu za mkononi. Hii inasababisha 22% ya jumla ya watu katika KJSA kutumia mtandao wa simu mwishoni mwa 2021 (na 40% ya watu wazima wa zaidi ya miaka 18) [16].
Ingawa faida na masharti ya Huduma za Utengamao Kidijitali zinatia matumaini, utekelezaji wa huduma hizo katika KJSA bado ni duni. Utafiti unapendekeza kwamba idadi kubwa ya mipango ya Afya ya Kidijitali ndani ya nchi za Afrika inasalia kuwa suala la kutafitiwa [17]. Utafiti mwingi wa Huduma za Utengamao Kidijitali katika eneo hili umekuwa na lengo la kutathmini ukubalifu wa wateja, familia zao na watoa huduma za afya katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, wakati ambapo bado kuna ukosefu wa mwongozo wa jinsi ya kutekeleza huduma hizi.
Katika sura hii, tunatoa muhtasari wa matumizi ya teknolojia za kawaida ambazo tayari zinatumika katika KJSA. Iwapo ungependa kupata teknologia nyingine zinazotumika katika huduma za utengamao, tazama sura ya 6 ‘’Teknolojia’’. Iwapo unavutiwa na mambo mengine ya teknolojia yanayochochea au kutatiza utekelezaji wa Huduma za Utengamao Kidijitali katika muktadha wa KJSA, tafadhali nenda kwenye sura ya 5.
Uingiliaji kati kupitia arafa unaonyesha kutumika zaidi katika Huduma za Utengamao Kidijitali katika muktadha wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika. Arafa zinaweza kutumika kupitia programu za WhatsApp au kwa simu ya rununu. Uingiliaji kati wa arafa mbalimbali umetathminiwa nchini Kenya, Nigeria, Uganda, Kameruni na Afrika Kusini [14,18-22]. Katika muktadha huu, arafa zilitumika kama ushauri wa kidijitali na kusaidia watu wa rika moja walio na VVU [19], kama ukumbusho wa tiba unaolenga kuboresha ufuasi wa tiba ya kisukari/msongo wa mawazo, kama kichocheo cha kukuza shughuli za kimwili [14,20,21], kama uingiliaji kati wa kidijitali unaolenga utambuzi wa wazee wanaopitia upweke [20], na kama elimu kwa mteja juu ya ujuzi wa ugonjwa na udhibiti wa glisemia [22]. Ingawa utumiaji wa arafa ulionekana kukubalika kwa watumiaji na umethibitishwa kuwa na mafanikio na ufanisi katika kuboresha matokeo ya afya [18,20,22] baadhi ya changamoto pia zilitambuliwa. Changamoto hizi ni pamoja na masuala ya kiufundi, kasi ndogo, ukosefu wa ujuzi wa kidijitali kwa wateja, tashwishi juu ya ufanisi wake, na gharama [14,18,22]. Ingawa changamoto hizi zilishughulikiwa katika tafiti hizi, hii inaonyesha kuwa hata suluhu za gharama nafuu zinaweza kuwa na changamoto. Kwa hivyo, ili kutekeleza suluhu rahisi za kidijitali kwa madhumuni ya huduma za afya katika nchi za Afrika, masuala ya kiufundi, kasi ndogo, ukosefu wa ujuzi wa kidijitali, tashwishi juu ya ufanisi na gharama hazipaswi kupuuzwa kwani haya yanaweza kutatiza utumiaji mzuri wa suluhu za kidijitali.
Wakati wa mradi wa RADIC, tulifanya mapitio ya upeo ili kutoa muktasari wa mbinu za Huduma za Utengamao Kidijitali ambazo tayari zimetekelezwa katika Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika. Kama hatua ya ziada ya kimbinu, tulijumuisha wadau ili kueleza zaidi kuhusu mada hiyo. Wakati wa mkutano, tuliomba wadau kutoa maoni yao kuhusu mbinu za teknolojia za Huduma za Utengamao Kidijitali zinazofaa zaidi katika Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika. Wadau hao walikuwa ni wataalamu wa Huduma za Utengamao Kidijitali (n=1), meneja wa mafunzo ya kielektroniki (n=1), walimu wa sayansi ya afya (n=2), weledi wa huduma za utengamao, mtafiti msaidizi (n=1) na wataalamu wa tibamaungo na wataalamu wa kazi kama watafiti (n=6). Wadau saba kati ya washiriki kumi na mmoja tayari walikuwa na uzoefu wa awali wa Huduma za Utengamao Kidijitali. Wadau wengi wanaamini kuwa arafa ni chombo chenye nguvu hasa vijijini kwa sababu hakihitaji muunganisho wa mtandao. Zaidi ya hayo, wadau hawa wanasisitiza kuwa arafa haitegemei sana kusoma na kuandika na hivyo hufikiwa na kutumiwa na watu wengi zaidi.
Programu zinazotegemea wavuti, na kongamanovideo pia hutumika kwa madhumuni ya huduma za utengamao nchini Ethiopia, Kenya na Afrika Kusini. Ingawa teknolojia hizi zinatumika kuboresha ufuasi wa tiba [23,24] na kutoa usaidizi rika kupitia gumzovikundi na jukwaa la kidijitali [25], pia hutumiwa kuingilia kati watu walio na mfadhaiko [26-28], wenye kiharusi [29] na watu walio na dalili za shinikizo la damu na uchovu wa kihisia [30]. Kwa ujumla, watumiaji waliridhika kushughulikiwa na kuhamasishwa kuzitumia, hivyo basi huduma za kidijitali zinaonekana kuboresha maisha [24] mfadhaiko [29] na hutoa gharama ndogo [24,28,31,32]. Kando na matokeo haya mazuri, pia kuna vizuizi, kama vile ujuzi mdogo wa mtandao kwa wateja na ukosefu wa ufikiaji wa vifaa vinavyofanya kazi.
Wadau hao wanaamini pia kwamba siku zijazo, programu zinazotegemea wavuti, na kongamanovideo zitakuwa ni teknolojia muhimu zaidi za huduma za utengamao katika Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika. Wanafikiria kwamba programu za simu ni muhimu sana katika kuongeza ushiriki wa huduma za utengamao. Ingawa matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa kongamanovideo linawezekana na linakubalika katika nchi za KJSA, kama bado halijatekelezwa.
Uchapishaji wa 3D bado hautumiki sana katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika ikilinganishwa na viungobandia vilivyotengenezwa viwandani. Teknolojia hii ibuka inaweza kupunguza muda wa uzalishaji vyombo vya viungobandia na hivyo kupunguza gharama.
Mpango mmoja uliotekelezwa nchini Uganda, Tanzania, Kambodia [33] ulihamisha vichapishaji vya 3D hadi eneo la mashambani ambapo viungobandia vilichapishwa moja kwa moja bila kupoteza wakati kwa ajili ya watu waliokatwa viungo. Ijapokuwa utendakazi wa viungobandia vilivyochapishwa vya 3D unafananishwa na viungobandia vilivyotengenezwa kienyeji, utumiaji wa viungobandia vinavyotengenezwa ni bora zaidi, vikundi vinavyohusika vinachukulia uchapishaji wa 3D kuwa muhimu kwa huduma za utengamao, kwani unaweza kupunguza gharama ya kutengeneza viungobandia.