1.4 Uwezo
Sehemu muhimu ya huduma ya afya kwa wote ni “kuhakikisha kwamba watu wote wanapata huduma muhimu za afya (ikiwa ni pamoja na ukingaji, ukuzaji, utabibu, huduma za utengamao na upunguzaji maumivu) kwa wingi na ubora wa kutosha ili kuwa na ufanisi, huku tukihakikisha kwamba matumizi ya huduma hizi hayamweki mtumiaji katika matatizo ya kifedha” [2]. Kimsingi, Huduma ya Afya kwa Wote, ina maana kwamba watu wote kila mahali wana uwezo wa kupata huduma za afya. Pia inaashiria mfumo dhabiti wa afya unaozingatia watu kulingana na huduma ya afya ya msingi. Shirika la Afya Ulimwenguni (2000) pia linasisitiza malengo matatu yaliyounganishwa.
- Fursa sawa katika kupata huduma za afya - wanaohitaji huduma hizo wanapaswa kuzipokea, sio tu wale wanaoweza kuzilipia.
- Huduma za afya ziwe bora na nzuri ili kuboresha afya ya wale wanaopokea huduma.
- Ulinzi dhidi ya hatari ya kifedha ili kuhakikisha kuwa gharama ya kupata huduma haiwaweki watu katika matatizo ya kifedha.
Kulenga huduma ya afya kwa wote ifikiapo 2030 kunalingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (MMEUM) 3.8 [3]. Mtazamo wa matumaini wa kutekelezwa kwa Huduma ya Afya kwa Wote duniani ni fursa zinazotokana na maendeleo ya haraka ya teknolojia ya kidijitali na kuenea kwa mtandao wa simu katika bara zima.
Kwa hivyo, tunafupisha uwezo wa Huduma za Utengamao Kidijitali kutokana na mitazamo ya wadau mbalimbali katika mfumo ambao ni muhimu katika Afrika Mashariki, angalia pia kielelezo 1. Kwa upande mwengine, Huduma za Utengamao Kidijitali zinaweza kuwa na manufaa kwa jamii na /au mfumo wa huduma ya afya. Kwa upande mwingine, zina athari kwa mteja, mlezi na /au wafanyakazi wa huduma za utengamao. Mtoa huduma ya afya pia anaweza kufaidika kutokana na utekelezaji wa Huduma za Utengamao Kidijitali.
Mteja: Faida kubwa ya Huduma za Utengamao Kidijitali ni uwezekano wake kwa watu walio mbali na hawawezi au hawataki kupata huduma za utengamao wa umma kwa hivyo hawapati usaidizi wanaohitaji [4]. Uwezekano wa huduma za utengamao unaweza kufanyika hata kama kuna ukosefu wa wafanyakazi wa afya, gharama kubwa za kifedha zinazohusiana na huduma za utengamao, hali duni ya usafiri au umbali wa kijiografia.
Aidha, ukosefu wa faragha katika vituo vya huduma za utengamao na hofu ya unyanyapaa, kupitia ufikiaji wa huduma za afya, vilevile, hupunguza matumizi ya huduma za utengamao. Hapa, kwa mfano, unaweza kufikiria programu ambayo hutoa mazoezi kwa mteja afanyie nyumbani. Mfano mwingine ni kutumia vikumbusho vya matibabu kupitia arafa ili kuongeza ufuasi na matokeo ya huduma za utengamao.
Faida zaidi ya Huduma za Utengamao Kidijitali ni upatikanaji wa habari hata nje ya mandhari ya kliniki. Teknolojia hutoa aina mbalimbali na unyumbufu wa kutumia taarifa za afya (tovuti, programu shirikishi, michezo, uhalisia pepe na uhalisia uliodhibitiwa, michanganyiko ya maandishi, picha, sauti na video, zana za mitandao ya kijamii, uhuishaji, vikokotoo hatari) ambavyo vinaweza kusaidia wateja kulinganisha mahitaji na mapendeleo yao ya kibinafsi.
Kwa kuongezea, matumizi ya teknolojia ya dijitali huwawezesha watu binafsi kudhibiti zaidi afya zao na kuwa na ufikiaji bora wa data zao wenyewe, huku wakibaki wameunganishwa na timu ya huduma ya afya [5-7]. Baadhi ya zana za kidijitali (kwa mfano programu, vifaa vinavyobebeka vilivyo na uhalisia ulioboreshwa) huwavutia wateja kwa vipengele vya kuburudisha na kuingiliana, ambavyo huvutia usikivu wa wateja, kuwashirikisha kimawazo na kihisia. Hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa ushiriki na ufuasi wa tiba [8].
Zaidi ya hayo, uingiliaji kati wa kidijitali mara nyingi hujumuisha mitandao ya usaidizi wa rika na jumuiya za mtandaoni ambapo wateja wanaweza kuungana na wengine wanaokabiliwa na changamoto zinazofanana. Vikundi hivi vya usaidizi rika hutoa nafasi salama kwa wateja kushirikishiana katika uzoefu wao, kutafuta ushauri, na kutiwa moyo, kupunguza hisia za kutengwa na kunyanyapaliwa.
Mtaalamu wa huduma za utengamao: Utekelezaji wa Huduma za Utengamao Kidijitali unamwesha mtaalamu wa afya, kwa mfano kufuatilia tabia ya mteja, ukubalifu, lishe, afya ya dijitali, kudhibiti dalili, au kufanya marekebisho ya haraka ya matibabu yaliyo mbali [9]. Zaidi ya hayo, suluhu za dijitali zina uwezo wa kuboresha mawasiliano kati ya mteja na mtaalamu wa afya, kwa sababu zinamwezesha mteja mwenyewe kutoa taarifa ya kibinafsi na kupata matibabu.
Mtoa huduma ya afya: Teknolojia za kidijitali zinaweza kusaidia usimamizi wa mtoa huduma ya afya kwa kutoa michakato ya nje kama vile usajili na/au malipo. Fikiria, kwa mfano, mteja ambaye anataka kuweka miadi katika hospitali au kufanya mazoezi. Mteja anaweza kujiandikisha kupitia jukwaa la mtandaoni na, baada ya kuongeza maelezo yake ya kibinafsi, anaweza kupata msaada unaotakikana.
Mfumo wa huduma ya afya: Huduma za Utengamao Kidijitali pia zina nafasi ya kupunguza gharama kwa mteja na mfumo wa huduma ya afya [10-12] kwa mfano vikao vya ana kwa ana na kusafiri kwenda katika vituo vya huduma za afya kunaweza kupunguzwa.
Kwa kuongezea, tafiti zingine zinaonyesha kuwa Huduma za Utengamao Kidijitali huboresha matokeo kwa wateja wanaougua kusita kwa moyo, kisukari, na magonjwa ya kupumua. Pia husaidia wateja kudhibiti maumivu, kuongeza shughuli zao za kimwili, na kuboresha afya ya akili, ubora wa chakula, na lishe. [13].

Kielelezo cha 1: Uwezo wa Huduma za Utengamao Kidijitali kwa kila mdau