4.2 Umuhimu wa ufikiaji katika Afrika Mashariki

Ufikiaji kama ilivyoelezwa hapo awali inaafiki kuwa kila mtu ana fursa sawa ya kufaidika na huduma za utengamao, ambazo zinapaswa kuwa bila kujali kiwango cha mtu cha kusoma na kuandika, sifa zao za kimwili au tabia ya viungo vya mwili , eneo lao la kijiografia, uwezo wa kifedha. Hata hivyo, hii inaweza isiakisi hali ya sasa katika nchi zetu kama mataifa yanayoendelea na hasa zaidi kama Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani bado tunatatizika kupata huduma za afya kwa usawa (1,2).Huduma za utengamao kupitia teknolojia ya dijitali kwa sasa haziepukiki kwani kila pahali pana hali ya juu ya teknolojia (3,4). Ni jukumu la kila serikali ya kitaifa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati, zinazokubalika na zilizo nafuu kwa watu wote (5), na suala hili limeimarishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 ambayo yanalenga kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeachwa nyuma hivyo basi kuweza kupunguza ukosefu wa usawa na kufikia afya njema na ustawi kwa wote (6). Kwa hivyo nchi za Afrika Mashariki hazina budi kukubaliana na matarajio haya. Zaidi ya hayo, teknolojia ya kidijitali ina manufaa zaidi katika eneo hili ambayo yatasaidia kupunguza pengo la uhaba wa wafanyakazi wa afya na kupunguza umbali wa kijiografia wa kupata huduma za afya. Katika maeneo mbalimbali yanayopatikana, ni muhimu kulinganisha mtumiaji na aina ya teknolojia inayokubalika zaidi (kama ilivyoelezwa katika sura ya 6) ambayo itakidhi mahitaji yao ya huduma ya utengamao na kuwawezesha wataalamu wa huduma ya utengamao kufanya maamuzi sahihi kulingana na ukadiriajisimu na tathminisimu inayohitajika. Hii inaweza kuhusisha uboreshaji wa tafsiri katika lugha ifaayo zaidi inayoeleweka kwa urahisi au kuhusisha wataalamu ambapo ina maana kwamba mtu anahitaji kutambua wahusika ambao watafunzwa kuwasaidia kupitia mchakato wa huduma za utengamao.

Ufikiaji mzuri na rahisi kwa hivyo utakuza utiifu wa huduma za utengamao na hivyo kutoa taswira ya hali halisi katika nchi za Afrika Mashariki.